Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari Masuala Mbalimbali Yanayohusu Haki Za Wasichana Tanzania

Shirika la Msichana Initiative leo limetimiza miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake, Shirika hili lilisajiliwa chini ya wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Namba ya Usajili 00NGO/08380 tarehe 19/01/2016. Shirika hili limekua likifanya kazi katika Mikoa ya Dodoma, Tabora, Shinyanga, Arusha, Bagamoyo, Dar es Salaam, Lindi na Mara katika Wilaya ya Tarime lengo likiwa ni kutetea haki za wasichana ili kupunguza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo watoto wa kike ili kuwa na jamii endelevu inayojali usawa wa kijinsia.
Tangu Shirika la Msichana Initiative lianze kufanya kazi, tumeona jitihada mbalimbali katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki zake sawa na mtoto wa kiume, ikiwepo haki ya kusoma na kushiriki katika nafasi mbalimbali za maendeleo.
Upatikanaji wa elimu umekua bora zaidi wasichana wengi wameweza kuanza darasa la kwanza pia kwenye kutatua suala la ukatili wa kijinsia, serikali na wadau wengine wamekua wanatekeleza na kusimamia Mpango wa Taifa wa kumaliza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). Pamoja na mafanikio hayo msichana bado anakutana na changamoto nyingi zinazomfanya ashindwe kubaki shule na kusoma.

HALI YA HAKI ZA WASICHANA TANZANIA
• Wasichana 2 kati ya 5 wanaolewa kabla ya kufika umri wa miaka 18 (TDHS 2015/16)
• Wasichana 27 kati ya 100 wanapata ujauzito kabla ya kufika umri wa miaka 18 (TDHS 2015/16)
• Wasichana hukosa masomo kwa muda wa siku 4 hadi tano wakati wa hedhi na msichana 1 kati ya 10 huacha shule kabisa
• msichana 1 kati ya 4 wenye umri wa miaka 15-19 ni mama tayari (TDHS 2015/16)
• Wasichana 69,067 wa shule ya msingi na sekondari waliacha shule katika mwaka 2015 (BEST 2016)
• Wasichana wengi huacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo mimba na ndoa za utotoni
• Tunakaribia kufikia usawa wa jinsia kwenye uandikishaji wa wanafunzi, hata hivyo chini ya moja ya tatu (1/3) ya wasichana wanaomaliza shule ya msingi humaliza elimu ya kidato cha nne
• Pia tumeona kuendelea kuwepo kwa baadhi ya sheria ambazo zinabagua mtoto wa kike kuweza kufikia fursa mbalimbali ikiwemo elimu. Ikiwemo kutokuruhusu wasichana waliopata ujauzito kurudi shule na Sheria ya ndoa inayoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa chini ya miaka 18.

JITIHADA ZA MSICHANA INITIATIVE KATIKA KUTETEA HAKI ZA MTOTO WA KIKE
Msichana Initiative tumekua tukiweka jitihada katika kumuwezesha mtoto wa kike kwa sababu tunaamini wasichana ni lazima wajengewe uwezo wa kujiamini, kujitambua na kuzifahamu haki zao na kujua ni namna gani wanaweza kuzitetea pale wanapozikosa katika Jamii.
Katika miaka mitatu (3) tumeweza kuwafikia zaidi ya wasichana 14,214, Wasichana 10,102 tumewafikia kupitia Klabu zetu za shule za msingi na sekondari, (mkoa wa Dodoma 9467), (Dar es salaam 95), (Arusha 240), (Lindi 25), (Bagamoyo 300) pia tumeweza kuwafikia jumla ya wasichana 600 katika mkoa ya Tabora na Shinyanga yaani wasichana 300 katika mkoa Tabora na wasichana 300 katika mkoa wa Shinyanga kupitia majukwaa ya Msichana Cafe yanayowakutanisha wasichana kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika jamii na kutumia sauti zao kwa kuelimisha wasichana wenzao na Jamii kwa ujumla. Pia tumeweza kuwafikia wasichana 1,077 kupitia Ajenda ya Msichana hii ikimaanisha wasichana 577 tuliwafikia kwa mwaka 2017 na wasichana zaidi ya 500 kwa mwaka 2018.
Lakini pia tumeweza kuwafikia Wasichana 2200 katika Mkoa wa Dar es salaam, Singida, Tanga, Lindi na Iringa kupitia kampeni ya Namthamini ambayo tuliitekeleza mwaka 2018 mwezi wa tatu kwa kushirikiana na East Africa Radio na Television. Pia tumeweza kuwakutanisha na kuwajengea uwezo wasichana viongozi 200 kuhusiana na masuala mbalimbali ya uongozi, harakati na jinsi ya kujisimamia wenyewe na kujiamini katika kuanzisha vitu vyao binafsi kupitia jukwaa letu la FIRE SIDE CHAT pia tumeweza kugawa baiskeli 35 kwa wanafunzi. Baiskeli 25 tulizitoa mkoa wa Lindi katika Shule ya Sekondari Nangaru na baiskeli 10 katika Shule ya Sekondari Mwitikira iliyopo Dodoma Wilaya ya Bahi. Mwisho kabisa tumewafikia wanajamii zaidi ya 1000 kupitia mradi wetu Msichana Cafe unaowakutanisha wazazi, Vijana na Wasichana wenyewe kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wasichana pamoja na kutafuta suluhisho la kutatua changamoto hizo katika mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Bahi katika kata ya Msisi, Kigwe, Mundemu, Bahi Sokoni, Chipanga, Ibugule, Mwitikira, Chali, Chipanga na Mpalanga.

MATARAJIO YETU
Kwa Miaka minne ijayo tutaendelea kuongeza nguvu na kujidhatiti katika kuangalia sheria zinazomkandamiza mtoto wa kike kama vile kuhakikisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inabadilishwa na pia kuondoa ubaguzi kwa mtoto wa kike ili apate haki yake ya msingi ya kupata elimu lakini pia kuhakikisha mifumo yetu inalinda na kutekeleza sheria hizo kwa watoto wa kike kwa sababu tunaamini unapomuendeleza mtoto wa kike ni sawa na kuiendeleza jamii yake kwa ujumla.
Mwisho kabisa tungependa kuiomba serikali, jamii pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya jamii tushirikiane na tuongeze jitihada katika kuhakikisha tunamlinda na kumtetea mtoto wa kike ili aweze kutimiza ndoto zake.
Msichana Initiative ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi kwa kushirikiana na serikali, jamii pamoja na wasichana wenye umri kuanzia miaka 10-25, lengo likiwa ni kutetea haki za msichana hasa haki ya kusomakuw. Vile vile tunawajenga ili waweze kujiamini, kujitambua na kuzifahamu haki zao za msingi kwenye jamii na kujua ni namna gani wanaweza kuzitetea pale wanapokandamizwa.
Tunafanya hivyo kupitia Msichana klabu, Majukwaa ya Kijamii(Msichana Café), kusaidia uanzishwaji na ufanyaji kazi wa Timu za Ulinzi wa Mwanawake na Watoto(WCPC) pamoja na kuhamasisha mabadiliko ya sheria mbalimbali zinazomkandamiza na kumnyima haki mtoto wa kike.

Asante!
Rebeca Gyumi,
……………………
Mkurugenzi Mtendaji,
Msichana Initiative (MI)

Imeandaliwa na Idara ya Mawasiliano Msichana Initiative.
Kwa Maulizo na Ufafanuzi kuhusu Kazi zetu.
Wasiliana nasi kupitia;
Simu +255222774100 au +255767042581.
Barua Pepe, Msichanainitiatives@gmail.com