Blog

Tamko la wasichana katika kusherehekea siku ya mtoto wa kike duniani 11 Oktoba, 2023

Kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba dunia huadhimisha siku ya mtoto wa kike duniani. Siku hii inalenga kutambua na kusherehekea mafanikio ya wasichana na kuangazia changamoto zinazowakumba watoto wa kike ili ziweze kupatiwa suluhisho. Maadhimisho ya mwaka huu yatatimiza miaka 11 tangu siku ya mtoto wa kike ianze kuadhimishwa mwaka  2012.

Katika kusherehekea siku hii muhimu  mwaka huu, mashirika ya C-Sema, Flaviana Matata Foundation,  Msichana Initiative pamoja na Tai  yanaendesha Jukwaa la Ajenda ya Msichana (Yaani Girl Agenda Forum) yakilenga kuwaleta pamoja wasichana kutoka maeneo mbalimbali pamoja na wadau wa haki za wasichana ili kusherehekea mafanikio ya wasichana na kuleta pamoja sauti za wasichana kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili na kutafuta suluhisho.

Ajenda ya Msichana ni mkutano wa kila mwaka unaowakutanisha wasichana kutoka sehemu  mbalimbali na wadau wa haki za wasichana kusherehekea mafanikio ya wasichana na kuangazia changamoto mbalimbali zinazowakandamiza wasichana kushindwa kuonesha uwezo wao kikamilifu. Jukwaa hili huwaweka wasichana pamoja ili kupaza sauti zao katika kuangazia masuala yao na kutoa mapendekezo

Ajenda ya Msichana 2023 imebeba kauli mbiu ya “Mimi ni Nani?: Kubadili Tamaduni na Mazoea ili kujenga Kizazi cha Wasichana Wanaojiamini’’. Kauli mbiu hii imejikita katika umuhimu wa stadi za maisha kwa wasichana hasa stadi ya KUJITAMBUA, KUJIAMINI NA KUWA NA NDOTO KUBWA ili kujenga kizazi cha wasichana wanaoweza kusimamia maono yao na kujiepusha na vishawishi.

SHUGHULI NDOGONDOGO TULIZOFANYA KABLA YA AJENDA YA MSICHANA

Kabla ya siku hii muhimu sisi wasichana tulifanya shughuli mbalimbali katika maeneo ya Dodoma, Tabora, Pwani, Dar es salaam pamoja na visiwani Zanzibar ili kuwafikia wasichana wenzetu pamoja na kufikia jamii zetu kuzungumza kwa undani kuhusu kauli mbiu hii na kujadili changamoto mbalimbali zinazotuzuia kutimiza ndoto zetu. Wasichana tulioshiriki leo tunawakilisha wasichana wengi kutoka katika mikoa yetu ambao walishiriki katika shughuli ndogondogo tulizofanya kuelekea maadhimisho haya.

Shughuli hizi zilifanyika kwa njia ya midahalo, mabonanza ya michezo, nyimbo, maigizo pamoja na ngoma. Kupitia shughuli hizi tuliweza kufikia wasichana 1219 kutoka mikoa tajwa hapo juu.  Idadi hii inajumuisha wasichana walioko shuleni, wasichana wanaoishi vijijini, wasichana wa mjini, wasichana walioko nje ya shule pamoja na wasichana ambao ni manusura wa ukatili wa kijinsia. Kupitia shughuli hizi tulifanya mijadala na kuzungumza  kwa undani kuhusu umuhimu wa kujitambua, kujiamini na kuwa na  ndoto kubwa.  Kama wasichana tulijifunza namna ambavyo malezi na makuzi pamoja na mahusiano ya kijamii yanavyoathiri namna tunavyojiona kama wasichana.

Jamii zetu zimekuwa na mila na desturi potofu ambazo zinawapa wasichana nafasi ya pili baada ya watoto wa kiume. Mila hizi zimekuwa zikiendelea kuchochea mimba na ndoa za utotoni, ukeketaji, pamoja na ukatili wa aina mbalimbali ambao umetupelekea kutokuwa na mtazamo chanya kuhusu sisi wenyewe.  Katika shughuli tuliyofanya wilaya ya Bagamoyo , mkoa wa Pwani, msichana mwenzetu  alisema

 

“Najisikia kufungwa na tamaduni zetu,siku zote wanatuambia kwamba sisi dhaifu na hatuwezi kufanya kile ambacho wavulana wanaweza. Inanivunja moyo na kukatisha tamaa.”

Aidha katika ngazi ya familia baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwapa watoto wa kiume kipaumbele katika kupata fursa ya elimu huku wasichana wakilazimishwa kufeli mitihani ili waozeshwe.  Hii imepelekea wasichana wengi kuendelea kupoteza uwezo wao wa kujiamini na kupoteza ndoto kubwa walizonazo. Katika shughuli iliyofanyika wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, msichana mwenzetu alisema

Elimu ni muhimu kwetu sisi wasichana lakini jamii yetu inaelekeza rasilimali nyingi kwa ajili ya elimu ya wavulana tu. Tunajiona kama hatuna thamani na hatuwezi kufikia ndoto zetu baadaye.”

Msichana mwingine kutoka wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani alisema,

“ Jamii bado ina mtazamo hasi na uelewa mdogo katika maswala ya elimu hususan kwa mtoto wa kike. Hivyo kuwapelekea wasichana wengi kutokuwa  na muamko wa elimu”.

Tunatambua mchango mkubwa wa serikali yetu katika kuhakikisha tunapata elimu. Kupitia juhudi za serikali tumeona idadi ya wasichana wanaojiunga na elimu msingi wakiwa wengi zaidi. Hata hivyo bado kuna mdondoko mkubwa wa wasichana kutokana na changamoto mbalimbali kama vile umbali mrefu kwenda shule, umaskini, mimba za utotoni pamoja na ndoa za utotoni.  Kwa upande mwingine bado kuna sheria kama vile Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ambayo bado inatoa mwanya kwa wasichana kuolewa kabla ya kutimiza miaka 18.  Hii inachangia wasichana wenzetu kulazimishwa kufeli mitihani ili waozwe kwa kuwa wakiwa nje ya mfumo rasmi wa shule sheria haiwalindi. Katika shughuli iliyofanyika wilaya ya chalinze mkoani Pwani, Msichana mwenzetu alisema

“ Changamoto kubwa inayotukumba sisi watoto wa kike ni kuachishwa shule na wazazi kwa lengo la kutaka kuozeshwa kwa kuwa tukiwa wanafunzi sheria inatulinda tusiozwe .”

Tunaamini kupitia mkutano huu viongozi wetu pamoja na wadau wa haki za wasichana watatupa  suluhisho la changamoto hizi.

 

WITO WETU

  • Wadau wa haki za wasichana waendelee kutoa elimu katika jamii zetu kuhusu madhara ya mila na desturi kandamizi  ili watoto wa kike wasionekane dhaifu na kupewa nafasi ya pili katika fursa mbalimbali,bali wapewe haki sawa na  watoto wa kiume . Msichana mwenzetu kutoka Bagamoyo alisema:

“Najisikia kufungwa na tamaduni zetu,Siku zote wanatuambia kwamba sisi dhaifu na hatuwezi kufanya kile ambacho wavulana wanaweza. Inanivunja moyo na kukatisha tamaa.”

 

  • Pia tunaiomba serikali yetu na wadau wa haki za wasichana watambue mchango wa wasichana na wanawake viongozi wanaofanya vizuri katika jamii, ili sisi wasichana tupate mifano mizuri ya kuiga na kujifunza kutoka kwao. Msichana mwenzetu kutoka wilaya chalinze mkoani Pwani alisema: 

“Asilimia kubwa ya watoto wakike wanashindwa  kufikia ndoto zao  kutokana na kukosa wasichana ambao ni mifano mizuri ya kuigwa na walezi watakaoweza kuwasimamia na kuwapa mwongozo wa maisha yao.”

  • Tunaiomba Serikali yetu iendelee kuweka msisitizo na kipaumbele katika elimu ya stadi za maisha ili kujenga kizazi cha wasichana wanaojitambua, kujiamini na kuwa na ndoto kubwa. Hii itatujenga kuwa wasichana tunaojitegemea , wasuluhishi wa changamoto zetu wenyewe tunaoweza kujisimamia wenyewe.
  • Pia tunaiomba serikali yetu iweke msisitizo katika sera na sheria wezeshi pamoja na kufanya mabadiliko ya sheria zinazotunyima sisi wasichana nafasi ya kuonesha uwezo wetu. Ikiwamo Sheria ya Ndoa, 1971.
  • Tunawaomba Wazazi na walezi wetu waendelee kutulea katika misingi inayotujenga sisi wasichana kujitambua, kujiamini na kuwa na ndoto kubwa.

Ninaamini kwamba nina uwezo wa kufanya kitu kikubwa, lakini mzigo wa majukumu ya nyumbani na ukosefu wa fursa zakujitambua kunanizuia kutimiza ndoto zangu.Nataka kuwa na uhuru wa kujifunza, kukua na kufatilia ndoto zangu.”

Sambamba na hilo tunaomba wazazi wetu watujenge katika malezi na misingi mizuri kwa kuzingatia changamoto zitokanazo na kasi ya sayansi na teknolojia. Msichana mwenzetu kutoka Zanzibar alisema

“Asilimia kubwa ya wasishana wanapotoshwa na matumizi mabaya ya mtandao na simu janja, nawashauri wazazi kuacha kuwapa watoto wao simu za mikononi bila utaratibu maalumu”

  • Sisi wasichana viongozi tuendelee kujitambua na kuwa chachu ya mabadiliko kwa wasichana wenzetu ili kujenga jamii yenye wasichana wanaojitambua na wanaojiamini. Msichana mwenzetu kutoka  Zanzibar  amesisitiza kuwa

“ Kama wasichana inabidi tujitambue na tutambue madhara yatakayotutokea endapo tutakubali kuolewa mapema wakati bado wadogo’’.

Sambambamba na hilo  Mabinti wa shule inatupasa kuzingatia masomo kwanza na kujilinda na makundi mabayai, moja ya changamoto inayomkumba mtoto wa kike ni kujiingiza katika makundi mabaya yanayo weza mpotosha”

 

HITIMISHO

Tunashukuru waandaji wa jukwaa hili kwa kutukutanisha wasichana pamoja na wadau mbalimbali wa haki za wasichana ili kuleta suluhisho la changamoto zetu. Pia tunamshukuru Mgeni Rasmi,  Mheshimiwa Spika , Dr. Tulia Ackson kwa kutoa muda wake kuja kutusikiliza na kufurahia siku hii muhimu pamoja na sisi. Tunaamini hizi changamoto tulizozisema leo zitapatiwa suluhisho ili kutusaidia wasichana wa Tanzania kutimiza ndoto zetu.

 

Imetolewa na; –

Wawakilishi wa wasichana kutoka

  • Tabora
  • Dodoma
  • Pwani
  • Dar es salaam